Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa kujieleza Uturuki kutathminiwa

Uhuru wa kujieleza Uturuki kutathminiwa

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa David Kaye atafanya ziara rasmi nchini Uturuki wiki hii kwa mara ya kwanza ili kutathmini hali ya haki ya uhuru wa maoni na kujieleza nchini.

Mtaalam huyo aliyeteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kufuatilia na kuripoti juu ya ukiukwaji wa haki ya uhuru wa maoni na kujieleza duniani kote, amesema Uturuki inakumbwa na changamoto kadhaa kwa hivi sasa na kwamba lile jaribio la mapinduzi mwezi Julai lilikosolewa na watu binafsi katika wigo wa kisiasa nchini humo akilitaja kama kushambuliwa kwa taasisi za kidemokrasia na utawala bora. Lakini ameongeza kuwa kabla na baada ya jaribio hilo, nafasi ya kupaza sauti kwa wasomi, waandishi wa habari, wanasheria na wengine katika asasi za kiraia imekuwa chini ya vitishio. Hii ni miongoni mwa masuala muhimu atakayoyafanyia utafiti wakati wa ziara yake ikiwemo pia kukusanya taarifa juu ya uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari, wana harakati na wasomi, pamoja na hatua kuchukuliwa ili kuhakikisha mjadala wa umma nchini humo.

Bwana Kaye aliyeakwa na serikali ya Uturuki atakutana na wabunge, uongozi wa nchi hiyo, viongozi wa mahakama na wawakilishi vyama vya kiraia.

Mtaalamu huyo ambaye atawasilisha ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu na matokeo juu ya ziara yake na kutoa mapendekezo juu ya utekelezaji wa haki ya uhuru wa kujieleza nchini atakutana na waandishi wa habari siku ya Ijumaa Novemba 18 mjini Ankara. Ziara ya mwisho kufanywa Uturuki ilkuwa mwaka wa 1996 na mtaalam huru Abid Hussain.