Skip to main content

Fungu maalumu kupasua mawimbi ya mabadiliko ya tabia nchi katika bahari Afrika:COP22

Fungu maalumu kupasua mawimbi ya mabadiliko ya tabia nchi katika bahari Afrika:COP22

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi unaoendelea Marrakech Morocco leo Jumamosi umekuwa na mkuatno maalumu kuhusu masuala ya bahari.

Mkutano huo uliowaleta pamoja washiriki 400 wa ngazi ya juu kutoka kote ulimwenguni umejadili masuala ya bahari na mabadiliko ya tabia nchi na kutoa ahadi ya hatua madhiubuti za kuunga mkono malengo ya maendeleo endelevu hususani lengo namba 14 ambalo ni la uhifadhi na matumizi endelevu ya bahari na rasilimali za majini.

Kwa mujibu wa UNFCC bahari ni muhimu kimataifa katika kuendesha maisha hapa duniani. Ni mtumiaji mkubwa wa hewa ya ukaa , inameza joto na kuzalisha nusu ya hewa ya oxygen inayovutwa na binadamu.

Pia bahari inaendesha maisha ya watu wa mwambao na jamii za kwenye visiwa ambazo zinaiita bahari kuwa ni nyumbani huku zikiitegemea kwa kukidhi mahitaji yao ya lishe na kiuchumi pia.

UNFCCC inasema umuhimu wa bahari uliainishwa rasmi kwenye kikao cha 43 cha jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC kilichofanyika Nairobi Kenya mapema mwaka huu na kuamua kuandaa ripoti maalumu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na bahari.

Katika mkutano wa leo shirika la chakula na kilimo FAO , Bank ya Dunia na Bank ya Maendeleo ya Afrika wametangaza fungu maalumu la Afrika kwa ajili ya uchumi wa bahari unaohimili mabadiliko ya tabia nchi.

Fungu hilo la msaada wa kiufundi na kifedha litasaidia uchumi unaotegemea bahari Afrika na kujenga uwezo wa maeneo ya pwani kuhimilli mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mikakati maalumu ikitegemea malengo na vipaumbele vya kila nchi.

Mradi huo utakusanya kati ya dola milioni 500 na 900 na kutekeleza program za mabadiliko ya tabia nchi kwa kipindi cha mwaka 2017-2020.