Skip to main content

Baraza la usalama ziarani DRC na Angola

Baraza la usalama ziarani DRC na Angola

Ujumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa umewasili huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa ziara ukanda wa maziwa makuu itakayowapeleka hadi Angola.

Katika ziara yao ya siku nne ujumbe huo DRC unatarajiwa kuzuru Kinshasa,na Mashariki mwa nchi mjini Goma na Beni ambako hivi karibuni kumekuwa na maandamano na  machafuko yaliyoambatana na kuahirishwa kwa uchaguzi uliokuwa ufanyike mwisho wa mwaka, na  Joseph Kabila kuendelea madarakani hadi 2018 utakapofanyika uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari punde baada ya kuwasili, mwakilishi wa kudumu wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa balozi Ismael Abraao Gaspar Martins ambaye pia ni mjumbe wa msafara huo amesema..

(Sauti ya balozi Martins)

“Unahitaji amani ya kisiasa. Unahitaji kusikia wito wa jamii ya kimataifa na ndio maana tuko hapa. Na ujumbe wetu ni kwamba jamii ya kimataifa inataka kufanya kazi na wanacongo ili kufanikisha utulivu wa kisiasa.”

Watakutana na Rais Kabila, upande wa upinzani, asasi za kiraia, waziri mkuu na wabunge kujadili mambo kadhaa ikiwemo hali ya kisiasa.

Kisha wataenda Luanda Angola watakapokuwa na mazungumzo na Rais Jose Do santos ambaye ni Rais wa mkutano wa kimataifa wa maziwa makuu, waziri mkuu na bunge la nchi hiyo.