Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukaguzi mpakani sio tiketi ya kupuuza haki za waomba hifadhi-UNHCR

Ukaguzi mpakani sio tiketi ya kupuuza haki za waomba hifadhi-UNHCR

Uungaji mkono wa Muungano wa Ulaya kuongeza kwa muda udhibiti mipakani katika nchi tano wanachama hakuondoi ukweli kwamba waomba hifadhi bado wana haki, umesema Umoja wa Mataifa.

Kauli hiyo ya shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR imekuja baada ya uamuzi wa karibuni wa Muungano wa Ulaya kuendelea na masuala ya upekuzi mipakani nchini Austria, Ujerumani, Denmark, Sweden na Norway, wakati kundi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wakiendelea kuingia Ugiriki.

Kimsingi hatua hizo zinaondoa ruhusa ya kusafiri bila pasi kuingia nchi hizo ambazo ni sehemu ya nchi za Schengen. Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR William, shirika hilo linatambua haja ya kuwa na udhibiti wa miapaka kwa ajili ya usalama.

Lakini amesema hatua hizo hazibadilishi majukumu na wajibu wa nchi chini ya sheria za kimataifa na za Muungano wa Ulaya za kuwapa waomba hifadhi fursa ya kuomba malazi.

(SAUTI YA SPINDLER)

“Kuomba hifadhi ni haki ya msingi ya binadamu ambayo ipo kwenye sheria za kitaifa na za Ulaya na zinahitaji kuhakikishwa. Hivyo kila udhibiti wa mipaka uwe ndani ya EU au nje unahitaji kuruhusu haki hiyo kutekelezwa”

Muungano wa Ulaya umependekeza kwamba upekuzi mipakani uendelee kwa miezi mingine mitatu katika nchi hizo tano zilizoomba.