Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kichomi na kuhara vyaongoza kwa vifo vya watoto: UNICEF

Kichomi na kuhara vyaongoza kwa vifo vya watoto: UNICEF

Licha ya kwamba ugonjwa wa kichomi au Pneumonia na kuhara huzuilika kwa njia za gharama na zisizo na gharama , bado magonjwa hayo yanaua watoto  milioni moja na laki nne  kila mwaka,  limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Kwa mujibu wa ufatifi uliochapishwa kwenye ripoti iitwayo Mmoja ni wengi iliyowasilishwa  leo kwenye mkutano wa 22 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi  COP22 unaoendela mjini Marrakech Morocco, vifo vitokanavyo na kichomi na kuhara vyaweza kuzuiliwa kwa kunyonyesha mtoto ipasavyo, chanjo, huduma bora za afya na kupunguza uchafuzi wa hewa majumbani.

UNICEF katika utafiti huo imesema kichomi unasalia kuwa ugonjwa unaoongoza kwa vifo vya watoto walio na umri wa chini ya mika mitano ambapo mwaka jana pekee watoto milioni moja walifariki dunia ikiwa ni wastani wa mtoto mmoja katika kila sekunde 35.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Fatoumata Ndiaye amewaambia wajumbe wa COP22 kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya hewa chafuzi itokanayo na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa afya na maendeleo  ya mtoto kunakosababishwa na kichomi na magonjwa mengine.