Skip to main content

Mpango wa Aleppo upitishwe haraka kuepusha zahma- Egeland

Mpango wa Aleppo upitishwe haraka kuepusha zahma- Egeland

Majira ya baridi kali yakiwa yanasogea, mpango unaoungwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya mashariki mwa Aleppo nchini Syria ambako mapigano yameacha maelfu ya watu mashakani ni lazima upitishwe mapema.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi, mratibu wa kikao cha kikosi kazi cha kimataifa kuhusu Syria, Jan Egeland amesema hatua hiyo ni muhimu kwani mgao wa mwisho wa chakula ulikuwa unasambazwa kwenye maeneo yaliyozingirwa.

Hivyo amesema ana matumaini kuwa mpango ambao Umoja  wa Mataifa umewasilisha kwa pande kinzani kwenye mzozo huo ili kuwezesha misaada kufikia walengwa na pia kuwaondoa wagonjwa utapitishwa na pande zote ambazo ni serikali ya Syria, Urusi na vikundi vya upinzani.

(Sauti ya Egeland)

 “Matokeo ya watu kukosa msaada na vifaa yatakuwa mabaya sana. Siwezi kuwazia mazingira hayo! Wapi  na lini tutapata ridhaa ya kupeleka misaada? Sifahamu kwa kweli. Wiki hii au wiki ijayo lakini inatakiwa ifanyike mapeka kwa sababu kimsingi mgao wa misaada utakoma leo.”

Alipoulizwa na wanahabari jinsi kuchaguliwa kwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani kunaweza kuathiri vipi janga la Syria, mratibu  huyo ametaka kusiwepo na kuingiliwa kokote kwa mpango huo kutoka Marekani na pia Urusi.