Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi wa Kenya lawamani kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji-UM

Polisi wa Kenya lawamani kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji-UM

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa , limealaani machafuko yaliyoambatana na msako wa polisi dhidi ya watu waliokuwa wakiandamana kwa amani katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi Amina Hassan na taarifa kamili.

(TAARIFA YA AMINA)

Wataalamu hao wameitaka mamlaka ya nchi hiyo kuchunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na kukamatwa kiholela kwa waandamanaji na waandishi wa habari na kutaka wote waliohusika kuwajibishwa.

Watu hao walikuwa wakiandamana kupinga madai ya ufisadi unaofanywa na serikali wakati polisi walipotumia mabomu ya kutoa machozi na virungu kuwatawanya ambapo watu kadhaa wameripotiwa kuumia au kuwekwa rumande kufuatia tukio hilo la Novemba tatu mwaka huu.

Wataalamu hao wamesema kuingilia haki ya uhuru wa kuandamana kwa amani ni suala lisilosameheka na hasa pale ambapo waandamanaji wanadai uwajibikaji kutoka kwa serikali.

Wamesema hofu ni wakati wenyewe, ukizingatia kwamba imesalia chini ya mwaka mmoja kabla ya raia wa Kenya kuingia tena kwenye uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge hapo Agost 2017. Wameitaka serikali ya Kenya kuheshimu haki za waandamanaji katika siku zijazo na kuiasa kwamba watakuwa wakifuatilia kwa karibu mambo yanayoendelea.