Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wanaendelea kuuawa na kutekwa Mosul-UM

Watu wanaendelea kuuawa na kutekwa Mosul-UM

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, inaendelea kupokea taarifa mbali mbali kuhusu raia huko Mosul, Iraq na matukio ya kuhamishwa kwa lazima na kundi la kigaidi la ISIL ikiwemo kutekwa na mauaji yanayofanyika.

Kwa mujibu wa Ravina shamdasani msemaji wa ofisi hiyo amesema mnamo Novemba 4, kundi hilo limezilazimisha kuhama familia 1,500 kutoka Hammam al-alil hadi uwanja wa ndege Mosul. Ofisi hiyo pia ina taarifa za kupatikana kwa maiti lakini bado hawana uthibitisho wa kutosha. Kuna habari kuwa karibu watu 295 askari wa zamani wa vikosi vya usalama Iraq wametekwa kutoka maeneo yaTal Afar na Mosul na mpaka sasa hawajulikani waliko.

Mwezi huu wa Novemba kuna madai ya kutekwa mashehe 30 kwenye eneo dogo la Qayrawan wilayani Sinjar inashukiwa kuwa 18 kati yao wameuawa mjini Tal Afar. Msemaji huyo ameongeza kuwa Ofisi yao inachunguza ripoti kuhusu taarifa za makaburi ya pamoja. Bi Shamdasani akijibu maswali mengine amesema karibu wiki moja imepita jamii zikijaribu kurudi kwenye vijiji vyao na zinazuiliwa.