Skip to main content

Tuelimisheni jukumu la UNMISS- Baraza la wazee Sudan Kusini

Tuelimisheni jukumu la UNMISS- Baraza la wazee Sudan Kusini

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Ellen Margrethe Løj, amesisitiza kuwa ujumbe wake uko nchini humo kusaidia wananchi na si vingineyo.

Amesema hayo kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la wazee wa Sudan Kusini kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini humo, akisisitiza wito wa kutaka milio ya risasi ikome ili wananchi warejee kwenye maisha yao ya kawaida.

Amewaeleza wazee hao wa jamii kuwa Umoja wa Mataifa hauko Sudan Kusini kutwaa nchi hiyo, bali unalenga kusaidia kupatia suluhu changamoto zinazokabili nchi hiyo ili wananchi waishi kwa amani na utulivu bila kujali jinsia au makabilia yao.

Bi. Løj ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, amesema kadri ambavyo watatua haraka tofauti baina yao kwa njia ya amani, ndivyo jinsi wananchi wanaweza kuishi kwa amani.

Deng Macham ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo la wazee Sudan Kusini ameiomba UNMISS kuandaa warsha itakayobainisha dhima ya ujumbe huo katika mchakato wa amani na maridhiano nchini humo.

Amesema jukwaa la aina hiyo litaondoa fikra potofu na kuelimisha raia kuhusu nafasi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo.