Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde epusheni watoto na mashambulizi Syria- UNICEF

Chondechonde epusheni watoto na mashambulizi Syria- UNICEF

Mashambulizi dhidi ya shule yameendelea huko Syria, ambapo katika tukio la leo, shule ya awali imeshambuliwa na kusababisha vifo vya watoto wane na wengine ambao idadi yao haikutajwa, wamejeruhiwa.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto nchini Syria, Hanaa Singer amesema katika taarifa kuwa shambulio hilo limetokea kwenye mji wa Harasta, kilometa chache kutoka mji mkuu, Damascus.

Amerejea wito wa UNICEF wa kutaka pande kwenye mzozo wa Syria na wengine wenye ushawishi kuhakikisha wanapatia ulinzi wa watoto kipaumbele kwa mujibu wa sharia za kimataifa za kibinadamu.

UNICEF inasema katika wiki mbili za mwisho wa mwezi uliopita, kulikuwepo na mfululizo wa mashambulizi dhidi ya shule, mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watoto zaidi ya 30.