Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu ya miaka 400 inaonyesha tsunami bado ni tishio kote duniani

Takwimu ya miaka 400 inaonyesha tsunami bado ni tishio kote duniani

Hii leo tarehe 5 Novemba ikiwa ni siku ya maadhimisho ya kimataifa ya mara ya kwanza kuhamasisha dunia kuhusu athari za Tsunami, mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa upunguzaji wa hatari ya majanga Robert Glasser, ameonya dhidi ya kulegeza hatua, wakati huu ambapo kuna tishio la kimataifa la tsunami.

Akizungumza huko New Delhi, India katika mkutano wa ukanda wa Asia wa mawaziri wanaoshughulikia upunguzaji wa hatari ya majanga Bwana Glasser amenukuu ripoti mbili za hivi karibuni zinazoonyesha kuwa matukio ya tsunami yanaweza kutokea katika maeneo mengi duniani.

Hata hivyo amesema Ulaya na Amerika ziko hatarini sambamba na nchi zinazozunguka bahari ya India na Pasifiki.

Naye mwandishi mkuu wa moja ya tafiti hizo, Profesa Fumihiko Imamura amesema ni muhimu kuhamasisha dunia kuhusu athari za Tsunami na watu lazima waelewe cha kufanya na wapi pa kwenda mara moja kengele ya tahadhari inapotolewa.