Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Matthew chatumbukiza watoto Haiti kwenye shida

Kimbunga Matthew chatumbukiza watoto Haiti kwenye shida

Mwezi mmoja baada ya kimbunga Matthew kuikumba Haiti karibu watoto laki sita bado wanahitaji msaada wa kibinadamu huku wengi wanakumbwa na magonjwa, njaa na utapia mlo limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Rosemary Musumba na taarifa kamili.

(Taarifa ya Rose)

Kwa mujibu Marc Vincent mwakilishi wa UNICEF Haiti watoto hao zaidi ya nusu milioni maisha yao yako mbali sana kurejea katika hali ya kawaida, wengi hawana makazi, hawaendi shule na wako hatarini.

UNICEF hivi sasa inafanya kila liwezekanalo kusaidia watoto hao haraka iwezekanavyo, huku takribani 1000 wakihofiwa kuathirika na ugonjwa wa kipindupindu kwa mwezi mmoja uliopita.

Kwa ujumla kimbunga Matthew kimewaacha watu laki nane wakihitaji msaada wa haraka wa chakula, na watoto zaidi ya 112,000 wakiwa kwenye hatari ya utapia mlo uliokithiri.