Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni Mosul yasambaratisha watu 20,700

Operesheni Mosul yasambaratisha watu 20,700

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwenye taarifa yao kutoka Baghdad linasema watu 20,700 wakiwemo watoto 9,700 wamesambaratishwa tangu kuanza kwa mapambano ya Mosul, Iraq tarehe 17 Oktoba na wanahitaji msaada wa haraka.

Mkuu wa mipango kwenye shirika hilo Pernille Ironside amesema akina mama na watoto waliokimbia makazi yao wanawafika wakiwa wamechoka, wana vumbi, bila viatu na hawajui mustakhbali. Amengezea kuwa cha muhimu ni kwa jamii wanakofikia kuhakikishiwa usalama, wanapewa maji safi na lishe kwa watoto.

Watoto kati ya umri wa miezi 6 na miaka 15 wanapata chanjo dhidi ya polio na surua - wengi wao ikiwa ni mara yao ya kwanza. Pia watoto wanapimwa utapiamlo na kutibiwa ipasavyo ikiwemo huduma za kisaikolojia na baadaye kuhamishwa katika kambi ya dharura na kupewa makazi. UNICEF inaandaa mazingira ya watoto kujifunza kwa muda na shughuli za burudani katika kambi hizo.

Tangu mwezi Oktoba, shirika hilo tayari limesaidia familia zaidi ya 1,500 na kuwapa chanjo watoto dhidi ya ugonjwa wa polio.