Skip to main content

Keating akaribisha muafaka wa kupunguza machafuko Gaalkacyo

Keating akaribisha muafaka wa kupunguza machafuko Gaalkacyo

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Somalia Michael Keating leo amekaribisha muafaka wa usitishaji uhasama kwenye mji wa Gaalkacyo uliofikiwa huko Abu Dhabi baina ya Rais wa Puntland, Abdiweli Mohamed Ali “Gaas” na Rais wa Galmudug, Abdikarim Hussein Guled.

Muafaka huo unawabana Marais hao wawili kuhakikisha wanajizuia na vitendo na matukio yoyote yatakayochochea ghasia kupitia vyombo vya habari , kuwaunga mkono wakimbizi wa ndani wanaorejea nyumbani baada ya kutawanywa na machafuko, na kuchagua tume ya pamoja ya kusaka suluhu ya kudumu ya mgogoro.

Hatua hii imekuja kufuatia mkataba uliofikiwa na viongozi hao yapata mwaka mmoja uliopita mnamo Desemba 2015 ambao haujatekelezwa. Bwana Keating amepongeza jukumu la Emarati kuwezesha mkataba huo mpya na amewataka marais hao wawili kuchukua hatua haraka kuhakikisha unatekelezwa.