Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa Paris, ukianza tusisahau nchi zinazoendelea

Mkataba wa Paris, ukianza tusisahau nchi zinazoendelea

Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ukianza kutekelezwa kesho tarehe Nne Novemba, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim amesema sasa ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo lengo kuu la nyaraka hiyo.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Bwana Jim amesema ikiwa lengo ni kupunguza ongezeko la joto, ni vyema kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu kwenye nchi zinazoendelea hautachochea ongezeko hilo.

Amesema katika miaka 15 ijayo, uwekezaji huo utafikia zaidi ya dola trilioni 90, hasa nchi zinazoendelea hivyo ni lazima kuhakikisha unakuwa ni uwekezaji endelevu unaochochea ukuaji uchumi endelevu.

Sambamba na hilo amesema nishati mbadala nayo iwe ni kichocheo pamoja na kuwezesha nchi hizo kuwa na uwezo wa kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Kim amesema mkutano wa COP22 unaoanza Marrakesh, Morocco, uwe na ari kama iliyokuwepo Paris, mwaka jana.