Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya kuondoa vikosi Sudan Kusini, UM wasubiri notisi rasmi

Kenya kuondoa vikosi Sudan Kusini, UM wasubiri notisi rasmi

Serikali ya Kenya imesema kuwa itaondoa walinda amani wake wote kutoka Sudan Kusini.

Hii ni siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kutangaza kumuondoa madarakani mkuu wa vikosi vya ujumbe wa umoja huo nchini Sudan Kusini, UNMISS Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki.

Hatua ya kuondolewa Luteni Jenerali Ondieki inatokana na uchunguzi wa tume huru ulioonyesha kuwa hakukuwepo na mwongozo wa kutosha kudhibiti ghasia za mwezi Julai huko Juba ambapo watu 73 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Alipoulizwa na wanahabari hii leo New York, Marekani kuhusu uamuzi huo wa serikali ya Kenya yenye walinda amani zaidi ya Elfu Moja Sudan Kusini, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema..

(sauti ya Dujarric)

 “Kama ninyi, mimi nimeona taarifa hizo kupitia mtandao wa Twitter kabla sijafika hapa. Bado hatujapata taarifa kuhusu uamuzi huo. Bilas haka tunatambua mchango wa dhati wa askari na polisi wa Kenya huko Sudan Kusini katika ulinzi wa amani. Tunasubiri kupata notisi rasmi kabla ya kuzungumzia zaidi suala hilo. Lakini niongeze kuwa kuwa ripoti inazungumzia masuala mapana zaidi kuhusu UNMISS.”