Skip to main content

CAR acheni machafuko na mgawanyiko, kumbatieni umoja na amani:Eliasson

CAR acheni machafuko na mgawanyiko, kumbatieni umoja na amani:Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson yuko ziarani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR. Katika ziara hiyo ya siku mbili Bwana Eliasson anakutana na viongozi wa serikali, kuhutubia bunge, kutembelea kambi za wakimbizi wa ndani Mpoko, atakutana na viongozi wa kidini, na pia viongozi wa kijamii.

Pia atapokea taarifa kuhusu hatua za usalama ikiwa ni pamoja na upokonyaji silaha, na zoezi la kuwarejesha katika jamii wapiganaji wa zamani. Leo tayari ameshazungumza na Rais wa nchi hiyo bwana Touadéra, mjini Bangui na kutoa wito wa kuacha machafuko na kukuimbatia mshikamano na amani. Akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa Guira FM kuhusu ziara yake bwana Eliasson amesema

(SAUTI YA ELIASSON)

“Nimeanza ziara yangu na mkutano, mazungumzo muhimu na Rais Toadera, mkuu wa nchi na pia wajumbe wa baraza lake la mawaziri. Tumejadili hali ya usalama nchini, lakini pia kwa muktada wa maridhiano, upokonyaji silaha na hatua zingine za lazima. Ni muhimu kwangu kuwaambia wananchi wote wa CAR kwamba Umoja wa Mataifa uko upande wenu. Sasa hivi mko katika wakati muhimu kwa historia yenu, mna historia ya machafuko na mgawanyiko na ni lazima mshikilie na kufuata mkondo wa Umoja.”