Skip to main content

Wanahabari walindwe na wawe huru kufanya kazi yao- UNESCO

Wanahabari walindwe na wawe huru kufanya kazi yao- UNESCO

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji sheria ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, Umoja wa Mataifa umetaka nchi wanachama kuazimia upya ili kuweka mazingira huru na salama kwa wanahabari kufanya kazi yao.

Katika ujumbe wake, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Irina Bokova amesema maeneo mengi duniani, waandishi wahabari wanabinywa katika haki yao ya kuripoti kwa uhuru taarifa mbali mbali.

Amesema tangu mwaka 2006 zaidi ya waandishi wahabari 800 wameuawa wakiwa kazini, na visa ambavyo vimefikishwa mbele ya haki ni chini  ya asilimia Saba.

Bi. Bokova amesema ukwepaji wa aina hiyo wa sheria, unakwamisha uhuru wa kujieleza na haki za binadamu huku wanaotekeleza wakipata ari zaidi ya kukiuka sheria.

Kwa mantiki hiyo ametaka serikali kuwafikisha mbele ya sheria wavunja haki za wanahabari, huku akisihi mashirika ya kiraia, polisi na mahakama kuongeza juhudi za kuzuia visa hivyo.