Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya kupata chakula Paraguay kuangaziwa

Haki ya kupata chakula Paraguay kuangaziwa

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula Hilal Elver ataanza ziara yake ya kwanza kabisa nchini Paraguay tarehe Nne mwezi huu kukusanya taarifa juu ya utambuzi wa haki ya chakula nchini humo.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema wakati wa ziara hiyo atatathmini mafanikio na vikwazo vya nchi hiyo ili kuhakikisha haki ya kupata chakula cha kutosha inazingatiwa.

Bi. Elver amesema hiyo itakuwa ni fursa ya kuchambua juhudi muhimu za serikali za kupunguza utapiamlo na kuhakikisha kuna uhakika wa chakula kwa wote.

Ameongezea kuwa jambo ambalo angetaka kuona likipatiwa kipaumbele maalum ni wanawake na watoto kwa kuzingatia mambo ya upatikanaji, ufikiaji bora na uendelevu wa uhakika wa chakula na upanuzi mkubwa wa uzalishaji wa maharagwe hasa ikilenga pia kuuza nje bidhaa hiyo.

Wakati wa ziara yake ya siku saba, mtaalamu huyo maalum atakutana na viongozi waandamizi wa serikali, wawakilishi wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, wajumbe wa asasi za kiraia, wawakilishi wa kiasili, wawakilishi wa sekta binafsi na wanachama wa jumuiya katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Bi. Elver atazungumza na wanahabari kuhusu ziara hiyo tarehe 10 mwezi huu na atawasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za binadamu mwezi Machi 2017.