Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali yaendelea kuwa tete Allepo- UM

Hali yaendelea kuwa tete Allepo- UM

Vifo vya raia wakiwamo watoto nchini Syria , matumizi ya makombora ya ardhi na magari yaliyosheheni vilipuzi ni ishara kwamba pande kinzani nchini Syria zimeshindwa kutii sheria za kimataifa za kibinadamu na vitendo hivyo havivumiliki, umesema leo Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya umoja huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjni Geneva, mwishoni mwa juma lililopita kumekuwa na taarifa za kuvurumishiwa makombora kwa raia katika eneo lenye idadi ya watu wengi Magharibi mwa Aleppo, eneo lionalokaliwa na serikali.

Zaidi ya watu 30 wakiwamo watoto 10 wameripotiwa kuawa , makumi wakijeruhiwa, huku pia kukiwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa za familia kuyakimbia maeneo hayo kuelekea katika ngome za wapinzani.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa OHCHR

(SAUTI RAVINA)

‘‘Pande zote Aleppo zinaendeleza uhasama unaoathiri raia wengi na kujenga hofu kwa wale wanaoendelea kuishi mjini hapo. Mashambulizi dhidi ya hospitali, shule, masoko, miundombinu ya maji, maeneo ya kuuzia mikate sasa ni kawaida na yaweza kuongeza uhalifu wa kivita.’’