Uhamishaji raia kwa nguvu Iraq unaendelea-OHCHR

Uhamishaji raia kwa nguvu Iraq unaendelea-OHCHR

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR, imesema inasikitishwa na mfululizo wa matukio ya kuwahamisha raia mjini Mosul, Iraq kwa makusudi vitendo vinavyodaiwa kuanza kutendwa majuma mawili yaliyopita.

Msemaji wa ofisi hiyo Ravina shamdasani amewaambia wandishi wa habari mjini Geneva hii leo kuwa ofisi yake imepokea taarifa kwamba jana asubuhi kundi la kigaidi la ISIL, lilipeleka makumi ya malori na mabasi kusini mwa Mosul kwa lengo la kuhamisha raia 25,000 mjini humo.

Amesema kufuatia majibishano ya mapigano baadhi ya malori yalilazimika kurudi lakini baadhi ya mabasi yalifanikiwa kufika eneo liitwalo Abusaif lililoko kilometa 15 kutoka mji uitwao Hamam Ali.

OHCHR imesema inasikitishwa na vitendo hivyo na kuhofia usalama wa raia kama anavyofafanua Ravina Shamdasani.

( SAUTI RAVINA)

‘‘Tunazitaka pande katika mgogoro huu kuhakikisha kwamba sheria za kimataifa zinafuatwa kwa hakika hususani kanuni ya utofautishaji na umakini wakati wa mashambulizi. Umakini maradufu uzingatiwe ili kuepuka vifo vya raia na kuwajeruhi.’’