Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICRC imezindua video ya gharama za kutoheshimu mitakaba ya Geneva

ICRC imezindua video ya gharama za kutoheshimu mitakaba ya Geneva

Shirika la kimataifa la Hilali nyekundu (ICRC) leo limezindua video yenye kushtua na kuogopesha, kuhusu madhara kwa binadamu yanatokanayo na kupuuza mikataba ya Geneva ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Video hiyo ambayo ni kampeni pia ina lengo la kulelimisha kuhusu sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu.Video hiyo ya sekunde 60 “Ushindi kwa njia yoyote ile” ambayo imetumia matukio halisi ya kwenye vita kutoka kote duniani, inawachukua watazamaji kwenye safari kutoa ndondoti hadi kwenye zahma ya kibinadamu. Ni kampeni ngumu sana, inayogusa na ya aina yake kutoka ICRC.

Kwa mujibu wa Peter Mauer rais wa ICRC, mabomu hospitalini, mamilioni ya watu kutawanywa, na ukatili wa kingono vitani imekuwa karibu kama jambo la kawaida. Ameongeza kuwa madhila kwa watu katika vita sio kitu kipya tena, na dunia inafeli katika kulikabili hili.

Ameongeza kuwa hakuna nchi za kutosha , hakuna majeshi ya kutosha, hakuna makundi yenye silaha ya kutosha ambayo yanazingatia misingi ya haki za binadamu iliyopo kwenye mikataba ya Geneva, na pale sheria za kimataifa za haki za binadamu zinapokiukwa wote tunalipa gharama.

Amezitaka nchi zote duniani kuzingatia na kuheshimu mikataba waliyotia saini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.