Wamakonde wasio na uraia Kenya hatimaye wapewa vitambulisho

Wamakonde wasio na uraia Kenya hatimaye wapewa vitambulisho

Hatimaye watu wenye asili ya Kimakonde 6,000 sasa wataondokana na tatizo la kutokuwa na utaifa baada ya serikali ya Kenya kuwatambua na kuwapa vitambulisho, limesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR .

Kwa mujibu wa shirika hilo watu hawa ambao wazazi na babu zao waliwasili nchini Kenya mwaka 1936 kutoka Tanzania na Msumbiji, walikuja kufanya kazi katika mashamba ya katani na miwa na hawakurudi nyumbani, na kwa miaka mingi sasa wamenyimwa haki zao za msingi za kibinadamu, kwani hawakutambuliwa kama raia wa Kenya.

Katika taarifa ya UNHCR, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye alitoa ahadi ya kutatua tatizo hilo ifikapo Desemba 2016, amenukuliwa akisema "Niwieni radhi imechukua muda mrefu sana kuwapa haki kama wenzetu Wakenya. Leo ni siku ya mwisho mtaitwa wageni."

Naye Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filipo Grandi, leo amerejelea upya wito kwa nchi wanachama wa kukomesha ukosefu wa utaifa ambao bado unaathiri watu milioni 10 ulimwenguni kote.

Amesema ni miaka miwili sasa tangu kampeni ya #Ibelong kuanzishwa na kumekua na mafanikio makubwa, lakini mapigano yaliyokithiri yanaweka mafanikio hayo hatarini.

Kampeni hiyo ina lengo la kufuta ukosefu wa utaifa ifikapo mwaka 2024.