Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fanyeni maonyesho ya urithi wenu leo-UNESCO

Fanyeni maonyesho ya urithi wenu leo-UNESCO

Leo ni siku ya kimataifa ya urithi wa sauti na picha ambapo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limesema siku hii inatoa fursa ya kuongeza uelewa wa haja ya kukiri umuhimu wa nyenzo hizi na kuchukua hatua za dharura kuzihifadhi.

Mada kuu ya mwaka huu ni "Ni hadithi yako-usiipoteze", ambapo UNESCO inahimiza ulimwengu wote kusherehekea siku hii kwa kufanya maonyesho ya urithi wa vielelezo vyao kama mpango wa kimataifa wa kukuza thamani yake.

Imesema, nyaraka za vielelezo hutueleza maisha ya watu na tamaduni zao kote duniani, na ni thibitisho la kumbukumbu zetu na vinaakisi utofauti wetu wa kiutamaduni na kijamii, na vinaweza kutusaidia kuishi na kufahamu ulimwengu ambao sote tunashiriki.

Hivyo imetoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi, kuimarisha hifadhi za kumbukumbu hizi, ili kuhakikisha vinabakia na kufikiwa na umma na vizazi vijavyo.