Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waonya dhidi ya uharibifu wa makusudi wa urithi wa dunia

UM waonya dhidi ya uharibifu wa makusudi wa urithi wa dunia

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kitamaduni, Karima Bennoune, ametoa wito wa kuchukuliwa haraka hatua za kimataifa dhidi ya uharibifu wa urithi wa utamaduni. Akitoa mifano ya uharibifu huo kwenye kikao cha baraza kuu mjini New York Jumatano, amezitaja nchi za Afghanistan, Iraq, Libya, Mali na kusisitiza kwamba kuna haja ya baraza hilo kuchukulia uharibifu wa utamaduni kama suala la haki za binadamu.

Bi Bennoune amesema ili kuelewa changamoto ya kulinda urithi wa kitamaduni kama vile makaburi ya thamani, na maeneo takatifu – ni lazima kuelewa kwanza haja ya kulinda watu na haki zao. Amesema mashambulizi kwa urithi wa kitamaduni ni mashambulizi kwa haki za binadamu na misingi yao.

Mtaalamu huyo ameelezea mizizi ya uharibifu ikiwa ni pamoja na migogoro ya kutumia silaha, na mashambulizi ya kiholela yanayo shindwa kutofautisha vyombo vya kijeshi na miundombinu ya kiraia. Na amependekeza kwa mujibu wa viwango vya kimataifa kukabiliana na misimamo na itikadi kali, utengano na mitazamo ya kibaguzi na kudumisha mikakati muhimu kama vile elimu Utu, kuheshimu haki za binadamu na maendeleo ya kuvumiliana.

Bi Bennoune pia ameomba kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watetezi wa haki za binadamu.