Skip to main content

OCHA: Nigeria yakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu Afrika

OCHA: Nigeria yakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu Afrika

Nigeria inakabiliwa na mgogoro mbaya kabisa wa kibinadamu barani Afrika. Kauli hiyo imetolewa na naibu mratibu wa masuala ya kibinadamu na mratibu wa shirika la OCHA nchini humo Peter Lundberg.

Hivi sasa watoto takribani laki nne wanakabiliwa na njaa na raia wanakabiliwa na ukosefu wa maji safi, huduma za afya, ulinzi, elimu na hawana uhakika wa chakula.

Amesema jimbo lililoathirika zaidi ni Borno ambako machafuko ya kundi la Boko Haram yamezidisha madhila kwa wananchi. Jumuiya ya kimataifa na serikali ya Nigeria vinajitahidi kutoa msaada lakini OCHA inasema bado hautoshi.

Mpango wa usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2016 nchini Nigeria unaohitaji dola milioni 484, hadi sasa umefadhiliwa chini ya asilimia 37. Orla Fagan ni afisa habari wa OCHA nchini Nigeria

(SAUTI YA ORLA)

“Watu wamekimbia, wamezihama nyumba zao, kuna wakati mmoja kumekuwa na watu milioni mbili waliotawanywa , na watu wa jimbo la Borno ndio walioathirika zaidi, wengi wao wamekwenda kwenye nyumba za hifadhi, na kwa jamii zinazowahifadhi, lakini kuna idadi kubwa ya watu wanaokimbia Borno nzima. Na kuna eneo kubwa ambalo hatuwezi kulifikia kwa sababu za kiusalama.”

Ameongeza kuwa hali hiyo haistahiki hivyo

(ORLA CUT 2)

"Hali hii ni lazima ikome watu lazima waweze kuishi kwa amani, waweze kurejea katika hali ya kawaida na kuweza kuchunga familia zao kwa usalama, na waweze kumudu elimu na watoto wao wawe na afya.”