UNHCR mbioni kukabiliana na wimbi la wakimbizi Iraq

UNHCR mbioni kukabiliana na wimbi la wakimbizi Iraq

Harakati za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR za kupeleka zaidi ya tenti 7,000 katika kambi zitakazohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wanaotarajiwa kusambaratishwa na mapigano ya Mosul nchini Iraq bado inaendelea.

Akizungumza katika mahojiano na redio ya Umoja wa Mataifa, Bruno Geddo, Afisa wa UNHCR nchini Iraq amesema mji wa Mosul bado una watu zaidi ya milioni 1.2, na shirika hilo linajiandaa kupokea idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani katika kambi tano ambazo ziko tayari kuwapokea na nyingine sita bado zikitayarishwa.

Amesema uwezo wa shirika hilo kupokea wakimbizi ni mdogo, na wanategemea kuwapokea kwa hatua na kwa wakati tofauti, kama ilivyopangwa katika mkakati wa kijeshi, na hiyo itakua bora zaidi katika usaidizi wa kibinadamu na rahisi kwa shirika hilo kumudu.

Amesema operesheni ya dharura ya kupeleka tenti hizo inatarajiwa kukamilishwa Jumamosi ili kuhakisha wapo tayari na walichohakikisha kabla ya kujenga makazi hayo ni ...

(Sauti ya Bruno)

"Sehemu ambapo makazi yamejengwa ni lazima yalindwe, ni lazima yawe mbali na mapigano ambapo hakuna uwezekano wa kombora kuangukia sehemu hiyo, na kuhakikisha hakuna mkimbizi wa ndani muIraqi atalipuliwa na bomu la ardhini , na ijengwe kwa kuzingatia ulinzi wao, ikiimanisha iwe na mwanga wa kutosha ili kupunguza matokeo ya ukatili wa kijinsia."