Vikwazo dhidi ya Cuba; Marekani yachukua hatua ya aina yake

Vikwazo dhidi ya Cuba; Marekani yachukua hatua ya aina yake

Baada ya kupinga mara 25 azimio la kusaka kuondoa vikwazo vya Marekani vya kiuchumi, kibiashara na kifedha dhidi ya Cuba, hatimaye leo Marekani bada ya kupinga imeamua kutoonyesha msimamo wowote huku nchi 191 zikiunga mkono azimio hilo.

Marekani na Israel mwaka jana zilipinga lakini hii leo azimio likiwasilishwa kwa mara ya 26, kwa pamoja hazikuonyesha msimamo wowote ambapo mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power ametaja sababu ya kubadilika kwa msimamo.

(Sauti ya Balozi Power)

"Leo Marekani haitapiga kura, hebu nieleze kwanini, mwezi Desemba 2014 Rais Obama aliweka wazi msimamo wake juu ya vikwazo. Wakati utawala wa Obama unakubali kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani kwa Cuba, ni wazi kwamba hatuungi mkono sababu za kuondolewa kwa vikwazo vilivyopo kwenye azimio hili. Lakini azimio lililopigiwa kura leo ni mfano halisi wa kwanini sera ya Marekani kwa Cuba ilikuwa haitekelezeki."

Awali akiwasilisha azimio hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bruno Eduardo Rodriguez Parrilla amesema vikwazo hivyo vimekuwa ahueni kwa Marekani huku vikizorotesha maisha ya wananchi wa Cuba, lawama ikitupiwa serikali.

Amesema licha Marekani kulegeza msimamo na hata Rais Barack Obama kutembelea nchi hiyo, bado hali si shwari hivyo amesema..

(Sauti ya Waziri Parrilla)

“Kuna baadhi ya watu wameniuliza ni kwanini nawasilisha azimio hili kwa mara nyingine kwa Baraza Kuu, siwezi kupuuza umuhimu wa kisiasa na kimaadili wa ujumbe ambao Baraza hili linatuma.  Hatua  ya kutoshiriki ambayo imetangazwa na Marekani ni hatua muhimu kwa mustakhbali wa kuimarisha uhusiano wa Marekani na Cuba. Tunatumai kwamba mazao yake yataonekana kwa vitendo.”