Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitendo vya kichochezi CAR havitarejesha nyuma azma yetu- Ban

Vitendo vya kichochezi CAR havitarejesha nyuma azma yetu- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ujumbe wa umoja huo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, MINUSCA utachukua hatua muhimu kwa mujibu wa mamlaka yake kuendelea kulinda raia na utulivu nchini humo.

Amesema hayo kufuatia ghasia za Jumatatu dhidi ya ofisi za MINUSCA zilizosababisha raia wanne kupoteza maisha huku watu 14 walijeruhiwa wakiwemo walinda amani watano.

Ban amelaani ghasia hizo huku akikaribisha hatua ya serikali ya CAR ya kuhakikisha waliosababisha kitendo hicho wanafikishwa mbele ya sheria.

Amesema vitendo vya wanaosaka kuvunja amani na utulivu nchini CAR havitayeyusha kazi nzuri inayoendelea ya kujenga uchumi na kuendeleza utengamano wa kijamii, bila kusahau mshikamano wa kimataifa.

Hivyo amesema ni matumaini yake kuwa mkutano wa wahisani kuhusu CAR utakaofanyika Ubelgiji tarehe 17 mwezi ujao utachochea usaidizi wa kimataifa kwenye maeneo muhimu nchini CAR.