Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM utawatendea haki watu wa Haiti:Eliasson

UM utawatendea haki watu wa Haiti:Eliasson

Umoja wa Mataifa umejizatiti kutenda haki kwa niaba ya watu wa Haiti, hasa linapokuja suala la athari zilizosababishwa na mlipuko wa  kipundupindu na kimbunga Matthew.

Hiyo ni ahadi iliyotolewa na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson , jumanne akisema hatua mbalimbali zitawasilishwa hivi karibuni , ili kusaidia kutokomeza mlipuko wa kipindupindu ambao unakadiriwa kuathiri Wahaiti 780,000.

Mahakama ya rufaa ya nchini Marekani hivi karibuni ilizingatia kinga ya Umoja wa Mataifa kutokana na kesi ya madai iliyowasilishwa kwa niaba ya waathirika, wakiulaumu Umoja wa Mataifa kwa mlipuko wa ugonjwa huo.

Akizungumza na Ari Gaitanis wa idara ya habari na mawasiliano ya Umoja wa Mataifa, Bwana Eliasson amesema Umoja wa Mataifa utafanya kila liwezekanalo kuwatendea haki watu wa Haiti

(SAUTI ELIASSON)

“Tunajitahidi sana kuhakikisha mikakati hiyo inakuwa tayari, kwa ajili ya Katibu Mkuu kuiwasilisha kwenye baraza kuu, mwezi ujao, inajumuisha kwanza mambo ya muhimu sana ya kuwasaidia watu wa Haiti kutokana na athari kubwa za kimbunga, pili ni hatua za kupambana na kipindupindu, hii inamaanisha matibabu, chanjo, kusaidia kuboresha masuala ya usafi na sekta ya afya, na huo ni mpango utakaogharimu takriban dola milioni 200. Na tunajitahidi kwa kila hali kukusanya fedha kwa ajili hiyo na tumepokea hatua nzuri kutoka benki ya dunia na benki ya maendeleo.”