Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani maauaji na ukatili Iraq

UM walaani maauaji na ukatili Iraq

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, imelaani mauaji yanayotekelezwa na kundi linalotaka dola ya kiislamu ISIL wakati huu ambapo jeshi la Iraq likiendelea kukaribia ngome ya wapiganaji wenye msimamo mkali ya Mosul.

Kwa mujibu wa taarifa ya OHCHR, habari ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa jamii zinazoishi karibu na mji ulioko kaskazini wamelazimishwa kuhamia karibu na wapiganaji magaidi ili watumiwe kama ngao.

Ofisi hiyo inasema Jumamosi ya Oktoba 22 wapiganaji wa ISIL wamedaiwa kuwaua wanawake watatau na watoto watatu wasichana kwa kuwafyatulia risasi, na kuwajeruhi wengine wanne, wakituhumiwa kuwa mbali mita 100 nyuma ya kundi lililokuwa likiburuzwa kuhamia eneo jingine.

Habari zinasema kuwa waathiriwa hao walikuwa wanasalia nyuma ya wenzao kwa kuwa mmoja wa watoto alikuwa ni mlemavu na ni miongoni mwa waliouawa.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takribani watu 10,000 wamefurushwa kutoka Mosul huku wengine 9000 wakiwa wamevuka mpaka kuingia Syria.