Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi Milioni 1.4 Haiti wahitaji msaada wa chakula

Wananchi Milioni 1.4 Haiti wahitaji msaada wa chakula

Umoja wa Mataifa na wadau wake katika miezi mitatu ijayo wanahitaji dola Milioni 56 ili kusaidia watu Milioni 1.4 nchini Haiti baada ya kimbunga Mathew kusomba mashamba na hata akiba ya chakula.

Kiwango hicho kinafuatia tathmini ya pamoja ya serikali ya Haiti na mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la chakula, FAO na lile la mpango wa chakula WFP ambayo imeonyesha kuwa kati ya watu hao, Laki Nane hali chakula mbaya zaidi.

Mathalani huko Grande-Anse, shughuli za kilimo zimesambaratishwa, halikadhalika mabohari ya vyakula, na kinachotegemewa zaidi hivi sasa kwa mlo ni matunda yaangukayo kutoka mitini.

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Amerika na Karibea Miguel Barreto amesema mazao ya kilimo yaliyoko sokoni punde yatamalizika na hivyo wanahitaji fedha ili kuendelea na mgao wa chakula na pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu ili waweze pia kujikwamua kimaisha.