Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita vya Sudan Kusini vinatia aibu

Vita vya Sudan Kusini vinatia aibu

Mwanariadha mkimbizi kutoka Sudan Kusini Kenyi Santino aliyewakilisha timu ya wakimbizi watano kutoka Sudan Kusini kwenye Olimpiki nchini Brazil, ametoa wito kwa taifa lake kuweka silaha zao chini, ili watoto wa Sudan Kusini nao wapate fursa ya kuwa wanamichezo nyota.

Kenyi Santino ametoa wito huo leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa, akisema wakati aliposhiriki michezo ya Olimpiki hakuna aliyejali kabila lake, na kilichokua muhimu kwake ilikuwa ni kubeba bendera ya nchi yake kwa mara ya kwanza katika michezo hiyo.

Amesema kinachowaleta pamoja watu wa Sudan Kusini ni kikubwa zaidi ya kile kinachowatenganisha, na ni aibu kuona nchi yake iliyopigania uhuru kwa zaidi ya miaka 30 bado iko vitani, akisema nchi yake ingekuwa haina vita basi...

(Sauti ya Kenyi)

"Ningefurahia ushabiki mkubwa kama ule walioupata wanamichezo wenzangu kutoka maeneo mengine duniani, labda hata ningeshinda medali kwa nchi yangu. Nataka kuamini kwamba hakutakua tena na vita nchini humu, kwani mahitaji ya vijana hayataweza kutekelezwa mpaka bunduki zitakapokua kimya."