Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha hewa ya ukaa chavunja rekodi 2015: WMO

Kiwango cha hewa ya ukaa chavunja rekodi 2015: WMO

Kiwango cha gesi joto angani kimefurutu ada mwaka 2015, wamesema wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya hali ya hewa , wakionya kwamba hali hiyo itasalia hivyo kwa vizazi vijavyo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO siku ya Jumatatu, matukio ya El Niño ndio yanayobebeshwa lawama kubwa kwa hali hiyo.

Ukame uliosababishwa na El Niño umeifanya dunia kushindwa kuhimili kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa ambayo inahusika na ongezeko la joto duniani.

WMO imeongeza kuwa mwaka 2015 ulighubikwa na hewa chafuzi ambayo imechangia katika mabadiliko ya tabia nchi, na kwa mara ya kwanza katika historia, hewa ukaa au CO2 imepindukia chembechembe 400 kwa kila milioni moja. Petteri Taalas, ni katibu mkuu wa WMO

(SAUTI YA PETTERI)

“Hivyo ni habari mbaya inapokuja hewa ya ukaa ni kwamba , ina maisha marefu sana na kurejea kwa viwango vya kabla ya viwanda kunaweza kuchukua maelfu ya miaka”

Takwimu za karibuni zinaonyesha viwango vya hewa ya ukaa sasa ni alimia 144 zaidi ya ilivyokuwa mwaka 1750.