Skip to main content

Matone mawili kubadili maisha ya watoto Iraq: UNICEF

Matone mawili kubadili maisha ya watoto Iraq: UNICEF

Ikiwa leo ni siku ya Polio duniani, mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF, la afya ulimwenguni WHO, kwa kushirikiana na wizara ya afya ya Iraq wamezindua kampeni ya juma moja ya kutoa chanjo ya polio kwa watoto nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF, kampeni hiyo inayoanikizwa na kauli mbiu matone mawili yaweza kubaidili maisha, itadumu kwa siku tano ikilenga kuwafikia watoto zaidi ya milioni tano walioko chini ya umri wa miaka mitano nchini Iraq bila kujali hadhi zao za chanjo za miaka iliyopita.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Iraq Peter Hawkins amenukuliwa akisema taifa hilo limedhamiria kuondoa Polio na tayari limeshaendesha kampeni 16  katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015 ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya Polio katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

UNICEF inasema tangu mwaka 2014 hakuna kisa kipya cha Polio kilichoripotiwa Iraq, mwaka jana nchi hiyo iliyondolewa katika orodha ya nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huo.