Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masharti ya usitishaji uhasama Yemen yazingatiwe: Cheikh

Masharti ya usitishaji uhasama Yemen yazingatiwe: Cheikh

Ismail Ould Cheikh Ahmed, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, amekaribisha kuanza utekelezaji wa usitishaji uhasama usiku wa kuamkia leo, na kuzitaka pande zote kuhakikisha masharti ya usitishaji uhasama yanaheshimiwa.

Mjumbe huyo maalum anatambua kuwa ukomeshaji wa uhasama ni tete lakini kwa kiasi kikubwa unaendelea na kusisitiza uboreshaji wa hali ya usalama kwa ujumla mjini Sana'a na maeneo kadhaa nchini Yemen licha ya kesi zilizoripotiwa za ukiukwaji katika maeneo mengine kama Taiz na kwenye mipaka na Utawala wa Saudi Arabia.

Amezitaka pande zote kujizuia na kuepuka kuchochea machafuko zaidi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanazingatia saa 72 ya usitishaji uhasama.Bwana Cheikh Ahmed anawasiliana na pande zote katika mzozo wa Yemen kuweza kuongeza muda wa usitishaji uhasama ili kuweka mazingira bora kwa ajili ya upatikanaji wa amani ya kudumu nchini humo.

Amezikumbusha pande zote masharti ya usitishaji uhasamani pamoja na kutozuia fursa za wahudumu wa misaada ya kibinadamu kufika sehemu zote za nchi hiyo.