Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji zaidi ya 300,000 wawasili Ulaya mwezi Oktoba: IOM

Wahamiaji zaidi ya 300,000 wawasili Ulaya mwezi Oktoba: IOM

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, limesema wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 300,000 wameingia Ulaya kupitia bahari katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka huu,wengi wao wakiwasili nchini Italia na Ugiriki.

Taarifa ya IOM imesema waliowasili Ugiriki ni zaidi ya 160,000 huku zaidi ya 145,000 wakiwasili Italia mwaka huu na kwamba idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na ile ya mwaka jana ambapo jumla ya wakimbizi na wahamiaji 650,000 walivuka kwenda Ulaya.

Shirika hilo limeongeza kuwa mwaka huu zaidi ya watu 3,500 wamefariki wakiwa wanajaribu kuvuka kupitia bahari, idadi hii ikiwa inajumuisha miili mitano iliyogunduliwa Jumatano baada ya meli ya Ireland kunusuru watu 118 kutoka Libya.

IOM kadhalika imesema inaendelea kuungaa mkono mpango wa Umoja wa Ulaya EU, wa kuwapatia makazi wahamiaji na wakimbizi kutoka Ugiriki na Italia katika nchi nyingine za umoja huo.