Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule haipaswi kuwa mtego wa mauti:UNICEF

Shule haipaswi kuwa mtego wa mauti:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema zaidi ya watoto milioni 1.7 hawaendi shule na wengine milioni 1.3 wamohatarini kuacha shule kutokana na vita vikali nchini Syria.

Katika ripoti yake ya leo, UNICEF imesema tangu kuanza kwa mapigano mwaka 2011 shule 4,000 zimeshambuliwa, na walimu 151,000 wameacha kazi.

Akizungumza na wandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema kila siku watoto wanahatarisha maisha yao wakienda shule, na sio hilo tu, bali pia...

(Sauti ya Christophe)

" Shule moja kati ya tatu nchini Syria haitumiki kwa sababu imeharibiwa, au inatumika kuhifadhi wakimbizi wa ndani au zinatumiwa na wapiganaji".

Amesema kampeni ya UNICEF ya kurejesha watoto shule iliyoanzishwa mwezi Septemba imeleta mafanikio, lakini vita vinazorotesha maendeleo ya kampeni hiyo.

Kwa mantiki hiyo, ametoa wito kwa wadau katika mzozo kuwalinda watoto, shule na raia na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.