Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya nguvu na ukwepaji sheria vimetawala DR Congo:UM

Matumizi ya nguvu na ukwepaji sheria vimetawala DR Congo:UM

Polisi, vikosi vya jeshi na askari wa ulinzi walitumia nguvu kupita kiasi ikiwemo silaha za hatari wakati wa maandamano mjini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, mwezi uliopita ambapo watu 53 waliuawa, 143 kujeruhiwa na zaidi ya 299 kukamatwa , imesema ripoti ya uchunguzi wa awali ya Umoja wa Mastaifa iliyotolewa leo. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Uchunguzi huo uliofanywa kwa pamoja na ofisi ya haki za binadamu ya mpango wa Umoja wa mataifa nchini DRC MONUSCO, imeorodesha wahanga 422 wa ukiukwaji wa haki za binadamu ukijumuisha haki ya kuishi, uhuru na usalama wa watu, uhuru wa kukusanyika kwa amani na kujieleza. Watu 48 kati ya 53 waliopoteza maisha waliuawa na vyomvo vya serikali ikiwemo polisi na 38 miongoni mwao walipigwa risasi kichwani, kifuani na mgongoni. Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva.

(SAUTI YA RAVINA) 

"Ukwepaji wa sheria kufuatia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo, kupiga risasi, kukatakata na ukamataji wa kiholela imekuwa ni janga kubwa nchini DRC kwa miongo mingi, hili linasikitisha na linaendelea kuchochea hali mbaya iliyopo sasa, licha ya kwamba idadi ya maafisa wa serikali wanafikishwa mbele ya sheria lakini visa hivyo vinaendelea kutekelezwa mara kwa mara."

Hata hivyo timu ya uchunguzi inasema visa vilivyoorodheshwa ni sehemu tuu kwani walinyimwa fursa ya kupata rekodi za serikali za vyumba vya kuhifadhi maiti na hospitali za umma ikiwemo sehemu mbili ambako maiti nyingi zilihifadhiwa.