Skip to main content

Maneno ya kuelezea janga la Syria yamekwisha- Ban

Maneno ya kuelezea janga la Syria yamekwisha- Ban

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu Syria ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-moon amewaeleza wanachama kuwa mzozo wa Syria unazidi kuchukua sura mpya ya kutisha kila uchao.

Amesema mashambulizi ya kutoka angani yanayoendeshwa na serikali ya Syria kwenye eneo la Aleppo tangu tarehe 23 mwezi Septemba yamekuwa ni ya mfululizo zaidi tangu kuanza kwa mzozo wa Syria takribani miaka sita iliyopita.

Idadi za vifo na majeruhi ni za kutisha, eneo la mashariki mwa Aleppo limezingirwa tangu Julai Saba na hakuna msafara wa Umoja wa Mataifa ambao umeingia.

Amerejelea onyo la mjumbe wake maalum Staffan de Mistura ya kwamba iwapo kasi ya sasa ya mashambulizi itaendelea, Aleppo itakuwa imesambaratishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Ban amesema hoja kuu ni lini jamii ya kimataifa itamaliza janga hilo na huku akisema..

“Nasikitika kuwa Baraza la Usalama limeshindwa kuwajibika kuweka amani Syria. Nataabishwa na suala kwamba uhasama wa kikanda umepatiwa kipaumbele badala ya mahtiaji ya wananchi wa Syria.”

Ban amesema maneno ya kuelezea hali ya Syria yamekwisha sasa ni kuazimia kushikamana na hatimaye kuleta amani kwa wananchi wa Syria na hivyo kuendeleza utu wa pamoja.