Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jimbo la Hirshabelle lakamilisha serikali, wadau wapongeza

Jimbo la Hirshabelle lakamilisha serikali, wadau wapongeza

Jumuiya ya kimataifa imekaribisha hitimisho la kuanzishwa kwa serikali yaj jimbo la Hirshabelle nchini Somalia na hivyo kuwa sehemu ya serikali ya shirikisho.

Pongezi hizo zimo kwenye taarifa ya pamoja ya Umoja wa Mataifa, ujumbe wa muungano wa Afrika Somalia, AMISOM, Muungano wa Ulaya, IGAD, Ethiopia, Sweden, Italia na Marekani.

Wadau hao wamepongeza rais wa serikali ya jimbo hilo Abdullahi Ali Osoble na makamu wake Ali Abdullahi Hussein kwa kuchukua usukani wa jukumu hilo nzito, wakitaka sasa wahakikishe wanajumuisha makundi yote ambayo hayakuwa kwenye mchakato huo kwa kutilia maanani maslahi ya jamii zote.

Halikadhalika wameitaka ijikite sasa kwenye mchakato wa uchaguzi wa bunge la shirikisho la Somalia.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating ambaye pia ni mkuu wa UNSOM amesema..

(Sauti ya Keating)

“Cha kufurahisha ni kwamba mpangilio huo umeongozwa na wasomali wenyewe na Umoja wa Mataifa na washirika wengine wamesaidia kifedha na kuwasaidia wao wenyewe kujiamulia na hii ndio kazi Umoja wa Mataifa imeitekeleza vyema.”