Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Libya bado ina jukumu la kujistawisha- Kobler

Libya bado ina jukumu la kujistawisha- Kobler

Libya bado ina jukumu kubwa la kuimarisha na kuanisha ushiriki wa maeneo yote nchini humo ili kuisaidia kuleta ustawi.

Hii ni kwa mujibu wa mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Martin Kobler ambaye amehutubia mkutano wa tisa wa mawaziri kutoka nchi jirani uliofanyika hii leo huko Niamey mji mkuu wa Niger.

Amesema ana wasiwasi kuhusu hali ilivyo mjini Tripoli, Libya, ambapo wajumbe wa serikali ya zamani walitwaa majengo ya baraza kuu la serikali akisema kitendo hicho cha kuunda mamlaka kando ya mamlaka kinakwamisha utekelezaji wa mkataba wa siasa nchini humo.

Bwana Kobler amesema baraza la urais nchini bado limekabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni kutokuwa na uwezo wa kuunda uongozi wa kawaida na kuimarisha mfumo mzuri wa utawala.

Ametaka kuboreshwa kwa usalama mpakani ili kuzuia uingizwaji wa silaha haramu ambapo inakadiriwa kuwa kuna silaha milioni 26 nchini Libya.

Amesema anatiwa moyo kwa kuanza kwa wiki ya kimataifa ya udhibiti wa matumzii ya silaha tarehe 24 mwezi huu, akisema itasaidia udhibiti wa silaha kwa kuwa silaha hazianguki kutoka hewani.