Saa 72 za usitishaji uhasama ni muhimu, lakini hazitoshi:UM

Saa 72 za usitishaji uhasama ni muhimu, lakini hazitoshi:UM

Usitishaji uhasama wa muda nchini Yemen umekaribishwa na wafanyakazi wa misaada wa Umoja wa mataifa, lakini wamesema hautoshi, wakati huu ambapo wahudumu wa misaada ya kibinadamu wakijaribu kufikisha msaada kwenye jamii zilizoghubikwa na machafuko na vigumu kuzifikia.

Usitishaji huo wa saa 72 utaanza rasmi usiku wa Jumatano ukishirikisha majeshi yanayomuunga mkono Rais Hadi Mansour na waasi wa upinzani wa Houthi.

Yemen ni moja ya nchi masikini sana duniani na vita vya miezi 18 vimekuwa na athari mbaya kwa watu wa taifa hilo limesema shirika la kuratibu masauala ya kibinadamu OCHA. Jamie McGoldrick, ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen.

(SAUTI YA McGOLDRICK)

“Kwa kuwa na saa 72 tu za fursa inaamanisha unaingilia mipango yako na kuelekeza msukumo kwengineko. Lakini kama tutakuwa na fursa katika maeneo hayo wakati wote, na tuweze kujipanga vinginevyo, tunaweza kusambaya vyema msaada.

Moja ya mambo muhimu wakati usitishaji uhasana ukianza kutekelezwa ni kufikisha msaada kwa watu kwenye mji wa Taiz, uko mstari wa mbele wa mapigano baiana ya serikali na waasi wa Houthi.

Watu laki sita wametawanywa na machafuko katikati mwa Yemen na Umoja wa Mataifa unasema kuwafikishia msaada wahusika ni changamoto kubwa. Huku uwanja pekee wa ndege unaofanya kazi umesambaratishwa na mashambulizi

(SAUTI YA MAcGOLDRICK)

"Hii inamaanisha kwamba meli zinachukua muda mrefu sana kufikisha misaada na kumekuwa na taarifa za mzigo kuachwa pwani kwa muda mrefu na wakati unaruhusiwa kufika unakotakiwa vitu vinakuwa vimeshaharibika”

Ili kulisaidia taifa hili Umoja wa mataifa umetoa ombi la dola bilioni 1.63 kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.