Kuondoa kabisa vikwazo Gaza ndio muarobaini- O’Brien

Kuondoa kabisa vikwazo Gaza ndio muarobaini- O’Brien

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya dharura, OCHA, Stephen O’Brien amesema mahitaji ya kibinadamu kwenye eneo linalokaliwa la wapalestina yanaendelea kuongezeka kila uchao.

Amesema hayo wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliokutana leo kwenye mjadala wa wazi kuhusu Mashariki ya Kati na hoja ya Palestina.

Amesema karibu kila mkazi wa eneo hilo ameathiriwa na mzozo utokanao na Israel kukalia eneo hilo ambapo umaskini na ukosefu wa ajira umesababisha robo ya kaya zote kukosa uhakika wa chakula, huku huduma za msingi kama maji zikisalia haba.

Bwana O’Brien ameshukuru hata hivyo Israel kwa kuuzia wakazi wa ukanda wa gazi mita Milioni 10 za ujazo wa maji lakini amesema hatua hiyo si endelevu.

(Sauti ya O’Brien)

“Iwapo tunataka mahitaji ya kibinadamu Gaza yapungue, tunahitaji kuweka shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi. Kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya pande nne, kuondolewa kabisa kwa vizuizi ni muhimu ili kupata maendeleo ya kudumu Gaza, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na azimio namba 1860 la Baraza la Usalama.”