Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya bei nafuu kuokoa watoto ulimwenguni:UNICEF

Chanjo ya bei nafuu kuokoa watoto ulimwenguni:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema sasa lina uwezo wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto ulimwenguni wanaofariki dunia kutokana na magonjwa hatari ya kuambukiza kama dondakoo, pepopunda, kifaduro, homa ya ini aina ya B na mafua. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(TAARIFA YA AMINA)

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha UNICEF, Bi Shannelle Hall, amesema uwezo huo unafanikishwa kutokana na ubia wa chanjo duniani GAVI na wadau wengine, ambao utaiwezesha UNICEF kupata chanjo moja tu yenye kuzuia magonjwa hayo matano ijulikanayo kama Pentavalent, kwa senti 87 kwa chanjo, ambayo ni nusu ya bei inayolipwa sasa.

Amesema UNICEF itanunua dozi milioni 450 mwakani na kuzipeleka katika nchi 80,ili kuokoa maisha ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano katika nchi masikini zaidi, ambao hufariki dunia kwa asilimia kubwa kutokana ukosefu wa ufadhili wa chanjo. Bi Shannelle anaongeza

(Sauti ya Shannelle)

" Ni kwa mara ya kwanza kabisa katika historia tuna soko la chanjo za bei nafuu ambapo nchi zinazojifadhili na zinazofadhiliwa, zote zina fursa sawa, hii ni muhimu, kwanza katika upatikanaji wa chanjo lakini pia kuweka shinikizo katika bajeti za kitaifa".