Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 22 zaihitajika kupambana na kipindupindu Yemen

Dola milioni 22 zaihitajika kupambana na kipindupindu Yemen

Shirika la afya duniani WHO na washirika wake wanahaha kusaka haraka mamilioni ya dola kutoka jumuiya ya kimataifa ili kudhibiti mlipuko wa kipindupindu nchini Yemen.

Jumla ya dola milioni 22.35 zinahitajika kwa ajili ya masuala ya afya, maji na usafi, na milioni 16.6 kati ya fedha hizo zinahitajika haraka.

Kufikia tarehe 17 mwezi huu kumekuwa na jumla ya visa 340 vinavyoshukiwa na kuarifiwa na 18 kati ya hivyo vimethibitishwa kuwa ni kipindupindu katika miji ya Taiz, Al-Hudaydah, Aden, Al Bayda, Lahj, na Sana’a .

Wagonjwa wanapatiwa tiba hivi sasa na hakuna vifo vilivyoripotiwa kutokana na ugonjwa huo. Zaidi ya watu milioni 7.6 wanaishi katika maeneo hayo yaliyoathirika huku wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni tatu wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.