Uhakika wa usalama Aleppo ni lazima kabla ya kuingiza misaada:UM

18 Oktoba 2016

Wito wa serikali ya Urusi na Syria wa kusitisha mapigano kwa muda katika mji wa Aleppo haimaanishi kuanza kupeleka msaada katika mji huo.

Ni kwa mujibu wa msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Jense Laerke, akiongeza kuwa ili kuanzisha operesheni ya kupeleka misaada, ni lazima silaha ziwekwe chini na uhakika utolewe.

Amewaambia waandishi wa  habari mjini Geneva, Uswisi kuwa watu 275,000 bado wamenaswa mashariki mwa mji huo, wakiwa wameshuhudia mapigano makali miezi na miezi sasa.

(Sauti ya Laerke)

"Umoja wa Mataifa unasisitiza kwa wadau wa mapigano kuhakikisha usalama wa kuingia maeneo yaliyoathirika bila ya vikwazo, kupeleka msaada kwa wale walioathirika na kuokoa wagonjwa na majeruhi. Umoja wa Mataifa na washirika wake wako tayari kuendelea na uokoaji na matibabu ya haraka ili kuokoa maisha punde tu hakikisho la usalama litakapotolewa na pande zote. Umoja wa Mataifa una mpango maalumu wa kuokoa wagonjwa na majeruhi kutoka mashariki mwa Aleppo."

Bwana Laerke amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa haujashiriki katika mpango wa amani wa Urusi na Syria, mpango ambao unatarajiwa kuanza Alhamisi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter