Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watoto wanaowasili Lampedusa peke yao imefurutu ada:

Idadi ya watoto wanaowasili Lampedusa peke yao imefurutu ada:

Idadi ya watoto wanaowasili peke yao kwenye kisiwa cha Lampedusa, Italia imefurutu ada, limesema Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, hii leo.

Watoto 20,000 tayari wamewasili katika kisiwa hicho katika miezi tisa iliyopita, idadi hiyo ikizidi idadi iliyorekodiwa katika mwaka mzima uliopita.

UNICEF imesema kati ya watoto hao waliowasili kuna watoto watatu wachanga, ambapo wawili wamezaliwa katika boti kwenye bahari ya mediterenia na mwingine mmoja katika bandari ya Lampedusa.

Halikadhalika limesema katika safari hii hatari, idadi ya watoto wanaozama baharini haijulikani, na hiyo ni dalili ya jinsi hali ilivyo mbaya. UNICEF na wadau wengine wanatoa msaada wa haraka kwa watoto hawa, lakini idadi hii inazorotesha kasi ya msaada. Sarah Crowe ni msemaji wa UNICEF, mjini Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Sarah)

"Mara nyingi watoto hawa wanakuwa hawajulikani, hawadumiwi, hawasajiliwi, na hupotea na kuendelea na safari yao Ulaya bila ya ulinzi wowote".