Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza umaskini

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza umaskini

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza umaskini (IDEP) na kwa kuadhimisha miaka 24 tangu kuanzishwa siku hii Umoja wa Mataifa leo umesisitiza haja ya kutambua na kushughulikia hali ya kutengwa na udhalilishaji mkubwa wa watu wanaoishi katika umaskini. Rosemary Musumba na taarifa kamili

(TAARIFA YA ROSE)

Katika ujumbe wake maalumu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ni muhimu kuheshimu ahadi za kujenga maisha ya amani, ustawi na utu kwa watu wote akiongeza kuwa inatupasa kutambua kwamba chuki na ubaguzi vinakwamisha jitihada zetu. Amesema ili kumaliza umaskini, ni lazima kuheshimu na kutetea haki za binadamu za watu wote na kushughulikia hali ya kutengwa na udhalilishaji.

Huu ni mwaka wa kwanza wa maadhimisho haya tangu uzinduzi wa malengo ya maendeleo endelevu SDG's na ajenda ya mwaka 2030.

Makadirio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa licha ya mafanikio makubwa tangu mwaka 2002 - idadi ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini inazidi kushuka ambapo mtu mmoja kati ya watu 8 bado wanaishi katika umaskini uliokithiri, hii ikiwa ni pamoja na watu milioni 800 ambao hawana chakula cha kutosha, huku watu bilioni 2.4 hawana huduma za kuboresha usafi wa mazingira, watu bilioni 1.1 hawana huduma za umeme na watu milioni 880 wanaishi katika makazi duni mijini.