Skip to main content

Ban akaribisha makubaliano ya kupunguza gesi yaliyofikiwa Rwanda

Ban akaribisha makubaliano ya kupunguza gesi yaliyofikiwa Rwanda

Makubaliano kuhusu kumaliza hatua kwa hatua gesi ambazo huchangia ongezeko la joto duniani yaliyofikiwa na nchi 150 katika mkutano nchini Rwanda, yamekaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Makubaliano hayo ya kupunguza gesi zifahamikazo kama Hydroflurocarbons (HFCs)  yamefuatia marekebisho ya mkataba wa Montreal  uliolenga katika kulinda mazingira dhidi ya gesi angamizi.

Hydroflurocarbons (HFCs) hutumiwa zaidi  katika jokofu, viyoyozi na dawa za kunyunyizia zenye aerosol.

Katika taarifa kupitia msemaji wake, Ban amesema kuondoa matumizi ya gesi hiyo kutasaidia kudhibiti joto katika sayari dunia na kuongeza kuwa makubaliano hayo ambayo yataanza kufanya kazi mwaka 2019,  ni muhimu na yanaweza kupunguza hadi nusu nyuzi joto la dunia ifikapo mwisho wa karne.